KARIBU KATIKA JUKWAA HURU MAHSUSI KWA WASTAARABU


JUKWAA LA NONGWA NI JUKWAA HURU KWA WAPENDA AMANI, HAKI NA MAENDELEO YA MTU MMOJA MMOJA NA JAMII KWA UJUMLA..


JUKWAA LA NONGWA TUPO HURU KUPOKEA NA KUTOA HABARI KWA UMMA AILIMURADI HATUMKWAZI MTU NA PIA TUNAZINGATIA ZAIDI UKWELI NA UWAZI.

JUKWAA HILI LIMEASISIWA NA NDG.NORBERT AMELIKA NONGWA, NI MWANAHARAKATI MZALIWA WA KIJIJI CHA KIPINGO-MALINYI ULANGA MKOANI MOROGORO.


WANA MOROGORO NA ULANGA HUSUSANI MALINYI NA TARAFA JIRANI HAPA NI UWANJA MAHSUSI KUJITAFAKARI WAPI TUMETOKA? WAPI TULIPO? TUNAELEKEA WAPI?NA KWA NAMNA IPI TUNAWEZA KUFIKA......? TIMIZA WAJIBU WAKO NDANI YA JUKWAA HILI nongwasjukwaa.blogspot.com




KARIBUNI WATANZANIA WOTE.




SISI TUNAAMINI "Umoja ni Nguvu"



JUKWAA LA NONGWA

Monday, March 14, 2011

IJUE WILAYA YA ULANGA

HALMASHAURI YA WILAYA ULANGA
 

 

 
                           

   
   
 
Utangulizi
 
Wilaya ya Ulanga ipo kusini mwa Mkoa na ya kwanza kwa ukubwa kimkoa yenye eneo la kilometa za mraba 24,560 ambazo ni sawa na hekta 2, 456,000 pia Wilaya ni ya sita kwa ukubwa kitaifa. Wilaya ipo Kusini mwa Mkoa huu, kwa upande wa Mashariki imepakana na Wilaya ya Liwale katika Mkoa wa Lindi. Upande wa Kusini imepakana na Namtumbo katika Mkoa wa Ruvuma na Kaskazini Wilaya jirani ya Kilombero. Makao Makuu ya Wilaya ni Mahenge ambao upo umbali wa kilomita 312 kusini mwa Mji wa Morogoro
 
 
UMBILE LA ARDHI
 
Wilaya ya Ulanga ina ukubwa wa kilomita za mraba 24,560 ambazo ni sawa na hekta 2,456,000. Kati ya eneo hili, 75% ni pori na misitu. Mbuga kubwa ya wanyama ya Selous ipo katika eneo hili. Kiasi cha hekta 614,000 ambayo ni 25% ya ardhi yote inafaa kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kilimo. Hata hivyo, hadi sasa inakadiriwa kiasi cha hekta 50,000 (8.1%) hadi 80,000 (13%) tu ndizo zinazolimwa. Fursa ya eneo la kilimo cha umwagiliaji ni zaidi ya hekta 9,470 kati yake hekta 175 (1.8%) zipo katika kilimo cha umwagiliaji. Wilaya inayo mito 40 kati ya hiyo, mito 34 inatiririka mwaka mzima. Kati ya mito inayotiririka mwaka mzima, 17 inatiririka kwenye mabonde yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji.



Mvua na joto
Wilaya ya Ulanga hupata mvua nyingi katika misimu miwili. Msimu wa Vuli kuanzia mwezi Oktoba hadi Januari na msimu wa Masika huanza mwezi Machi hadi Mei. Viwango vya mvua katika wilaya ni wastani wa milimita 800 hadi 1,600 kwa mwaka.

Wilaya ya Ulanga ina fursa kubwa kwa mapinduzi ya kijani ya kilimo kutokana na kuwa na rutuba ya asili katika ardhi, hali ya hewa nzuri na uoto wa asili. Katika hali ya kawaida zaidi ya 95% ya wakazi wa Ulanga hutegemea kilimo kwa ajili ya ajira, chakula na biashara. Shughuli nyingine za kiuchumi ni uvuvi na ufugaji. Wilaya ya Ulanga inatumia ramani mbili za kitaalam kutoka Kituo cha Utafiti wa masuala ya udongo cha Mlingano, Tanga. Ramani hizo ni “Soil and Physiography” na “Rainfed Crop Suitability”. Ramani hizi zinatoa maelekezo kuhusu aina ya mazao yanayostahili kulimwa katika wilaya.
Wilaya inazo kanda tatu za kilimo (Agro-ecological zones). Kwanza, kanda ya mwinuko ambayo ni sehemu za Tarafa ya Vigoi na Tarafa ya Mwaya (maeneo ya Sali). Pili, kanda ya mwinuko wa wastani ambayo ni sehemu za Tarafa ya Lupiro na Mwaya. Tatu, kanda ya tambarare inayojumuisha sehemu kubwa ya Tarafa za Mwaya, Mtimbira na Malinyi.
IDADI YA WATU

Kulingana na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2002, idadi ya watu Wilayani ni 193,280 (Wanaume 95,371 na Wanawake 97,909). Kwa mwaka 2008 Wilaya inakadiriwa kuwa na watu 221,103 (Wanaume 108,866 na Wanawake 112,237). Ongezeko la watu ni 2.4% kwa mwaka.
 
Utawala
Wilaya ya Ulanga ina majimbo mawili ya uchaguzi.Upande wa Magharibi ni jimbo la uchaguzi la Ulanga Magharibi na upande wa Mashariki ni jimbo la uchaguzi la Ulanga Mashariki Wilaya inayo Halmashauri ya Wilaya moja, iliyopo daraja la kwanza ambayo Mwenyekiti ni Mhe. Salum A. Mndembo na Mkurugenzi Mtendaji ni Bw. Alfred C. Luanda.
 
Sekta ya Kilimo
 
Katika hali ya kawaida wilaya ya Ulanga iko katika ukanda wa tropiki na hupata mvua mbili za misimu ya kilimo. Kwanza , mvua za vuli ambazo huanza kunyesha mwezi Oktoba hadi mwezi Januari. Mvua za masika ndizo mvua msimu mkubwa wa kilimo katika Wilaya na huanza kunyesha kuanzia mwezi Machi hadi Mei kwa wastani wa milimita 1200 hadi 1600 kwa mwaka.

Wilaya ya Ulanga ina hali nzuri ya ardhi, hewa na uoto wa asili. Wilaya ina eneo la hekta 614,000 zinazofaa kwa kilimo. Kati ya hizo hekta 9,470 zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji maji mashambani na hekta 604,530 zina fursa za kulimwa kwa kutegemea mvua. Inakadiriwa asilimia 19.ya eneo hilo sawa na hekta 115,869.8 zinatumika kwa kilimo.
Katika hali ya kawaida wakazi wa Ulanga zaidi ya asilimia 95 hutegemea kilimo kwa ajili ya chakula na biashara. Hata hivyo, bado sekta ya kilimo na mifugo inakabiliwa na changamoto muhimu ambazo zinakwaza maendeleo ya Kilimo katika wilaya. Agenda ya Mapinduzi ya Kijani ya Kilimo iliwekwa wazi kwa maafisa ugani, watendaji wa kata na vijiji, maafisa tarafa na wananchi wote. Lengo la Serikali ya Wilaya ya Ulanga ni kila kaya yenye nguvukazi lazima ilime angalau ekari mbili (2) ya mazao ya chakula na ekari mbili (2) mazao ya biashara na ekari moja zao la muhogo na viazi vitamu. Mazao ya muhogo na viazi vitamu yana uwezo wa kuhimili ukame na uhaba wa mvua.
Mwitikio wa wananchi na watendaji ni mzuri na wakuridhisha hasusan tarafa za Malinyi, Mtimbira na Lupiro . Kila kitongoji, kijiji, kata na tarafa wanafahamu agizo la Serikali ya wilaya. Hata hivyo, tathmini ya awali iliyoendeshwa kuhusu utekelezaji wa malengo ya kilimo sawa na wastani wa asilimia 62.5 ya malengo yaliyowekwa msimu wa
 


Upatikanaji wa pembejeo.
Matumizi ya mbolea kwa wilaya ya Ulanga ni kwa kiasi kidogo sana, mbolea mara nyingi huwa inatumika katika mazao ya bustani. Wakulima walio wengi wanaamini kuwa udongo wao una rutuba ya kutosha, wakulima wengi hutumia masalio ya mazao yao kurutubisha ardhi, pia wakulima walio wengi bado wanatumia mbegu zao za asili.
Idara ya kilimo imeendelea kuwaelimisha wakulima juu ya umuhimu wa kutumia mbegu bora, mbolea na viatilifu katika mashamba yao ili kuongeza tija kwa eneo kwa kutumia mashamba darasa. Katika jitihada za wilaya kubadilisha imani za wakulima juu ya matumizi ya mbegu bora na mbolea idara imeanzisha jumla ya mashamba darasa 6 katika tarafa ya Vigoi na Lupiro. Mashamba darasa hayo ni kwa ajili ya kilimo bora cha maharage, migomba, mpunga na vitunguu. Pia idara ina mpango wa kuanzisha mashamba darasa 20 ya mazao mbalimbali katika msimu wa kilimo wa 2008/2009


Ushirika na Masoko
 
Katika mwaka wa fedha 2006/07 serikali ilitenga wastani wa shillingi bilioni moja kwa kila mkoa kwa lengo la kuwawezesha wananchi wa kawaida vijijini na mijini kiuchumi, ili kuongeza ajira na kipato. Matarajio ya serikali ni kuwawezesha wananchi katika vikundi na mtu mmoja mmoja wanaojihusisha na shughuli za uzalishaji mali na biashara kupata mikopo yenye masharti nafuu itakayowapatia mitaji ya kujiendeleza katika shughuli zao na hivyo kujiondolea umaskini. Fedha hizo zitatolewa kupitia mfumo wa kibenki na mabenki yanayohusika na mpango huu ni NMB na CRDB kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa kutumia taratibu za kibenki.

Maendeleo ya Ushirika Wilaya ya Ulanga kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2005 hadi oktoba 2008.
Wilaya ya Ulanga ina jumla ya vyama vya Ushirika 54 vya aina mbalimbali ambavyo vipo hai, na kusajiliwa kwa Mujibu wa Sheria ya Ushirika Na. 20 ya mwaka 2003, kama ifuatavyo:
Vyama vya akiba na mikopo:
•  SACCOS za Kina mama 12
•  SACCOS za Vijana 1
•  SACCOS za Wafanyabiashara 1
•  SACCOS za Wafugaji/Wakulima 5
•  SACCOS za Wafanyakazi 3
•  SACCOS za Wakulima 30


•  Ushirika wa Wafugaji 2
Changamoto:
  • Elimu ya Ushirika, uwezeshaji na Ujasiriamali kutowafikia wote kwa wakati.
  • Mitaji midogo ya Saccos isiyokidhi mahitaji ya mikopo kwa wanachama.
  • Masharti magumu, na riba kubwa za mikopo toka Asasi za Kifedha.
  • Ukosefu wa rasilimali fedha na vitendea kazi kwa Maafisa Ushirika katika kusimamia ushirika Wilayani.
Mikakati:
  • Kuwa na Elimu ya Ushirika uwezeshaji na ujasiriamali endelevu msimu wa 2008/2010 kwa Vyama vya Ushirika.
  • Kuhamasisha wanachama kuchangia mitaji ili kuwa na Saccos imara Kiuchumi na endelevu msimu wa 2008/2010.
  • Kuendelea kushawishi Mabenki na Asasi za Kifedha kutoa mikopo kwa Saccos

Elimu
 
Utekelezaji wa Maendeleo ya Elimu Wilayani unaenda sambamba na utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi Wilaya ya Ulanga ina shule za msingi 92 za serikali zilizosajiliwa kati yake shule 85 zina madarasa ya Elimu ya Awali. Shule hizi zina jumla ya wanafunzi 2924 wa Elimu ya Awali wakiwemo Wavulana 1477 Wasichana 1447

Uandikishaji wa darasa la kwanza mwaka 2008 (Net Intake Ratio na Gross Intake Ratio)
Kwa mwaka 2008 Wilaya ya Ulanga ililenga kuandikisha watoto 8499 , wakiwemo wavulana 4269 na wasichana 4230 . Walioandikishwa ni wavulana 4342 na wasichana 4023 Jumla 8365. Hii ni sawa na asilimia 98% ya waliolengwa waliotazamiwa kuandikishwa shule darasa la kwanza.

 
Elimu ya Awali

Shule za awali ziko 140 na zina jumla ya watoto 6,940 kama ifuatavyo:
Mwaka wa 1
Mwaka wa II
Wav Was Jumla Wav Was Jumla
2,172 2,143 4,315 1,259 1,366 2,625
Elimu ya Msingi

Wilaya ya Kilombero ina shule za msingi 150. Kati ya shule hizo tatu (3) ni za Watu Binafsi nazo ni Lupa na Kapolo zilizopo Ifakara Mjini na Papango iliyopo katika mji mdogo wa Mlimba. Shule hizo tatu za binafsi hutumia lugha ya kiingereza kama lugha ya kufundishia. Shule hizo zina jumla ya wanafunzi 82,651 wakiwemo wavulana 41,912 na Wasichana 40,739.
 


Elimu ya Sekondari
Wilaya ina jumla ya Kata 24, Kata 20 zina Shule za Sekondari na Kata 4 hazina Shule za Sekondari. Kata za Lupiro na Vigoi zina shule 2 kila moja na Kata ya Malinyi ina Shule za Sekondari 3. Kata zisizo na Shule za Sekondari ni Kilosa kwa Mpepo, Sali, Msogezi na Lukande. Kata hizi hazina Shule za Sekondari kutokana na idadi ya wanafunzi wanaomaliza kuwa ndogo kuweza kukidhi kuwa na Shule za Sekondari, hivyo wanafunzi wanaofaulu wanapelekwa katika shule zilizopo kata ya jirani.
Wilaya imeteua shule tano (5) za Igota, Nawenge, Kipingo, Mtimbira na Mwaya kuwa na kidato cha tano na sita ili kukabiliana na wimbi la wanafunzi watakaohitimu kidato cha nne miaka miwili ijayo. Hivi sasa wilaya inaendelea kuboresha miundombinu katika shule hizi ili ifikapo 2011 ziweze kukidhi mahitaji ya kupokea wanafunzi wa kidato cha tano.
 
Maji
Katika kipindi hiki cha Awamu ya Nne Idara ya Maji imeweza kutekeleza miradi ya maji ya mtiririko ya bomba na yale ya chini ya ardhi ambayo ni ya visima vifupi vya maji.
Shughuli zilizotekelezwa katika kipindi cha mwaka miaka mitatu ya utawala wa awamu ya nne ni kama ifuatavyo:-

Utafifi na Ujenzi wa Visima vifupi

Utafiti wa visima vifupi 56 umefanyia katika vijiji 22. Baada ya utafiti na upimaji wa ubora wa maji kwa matumizi ya binadamu visima vifupi 40 vimechimbwa na kujengwa katika vijiji 18.
Ujenzi wa Skimu za Maji ya bomba.
Ujenzi wa Skimu ya maji mtiririko 1 ya Itete umekamilika, ambao unahudumia watu wapatao 18,600 wa Vijiji vya Minazini na Njiwa.
Aidha mradi wa maji ya bomba wa Sofi Majiji ujenzi wake unaendelea. Pamoja na ujenzi wa miradi hii, ukarabati wa skimu 3 za ruaha/Mzelezi, Sali na Mtimbira umefanyika, ambapo vituo 62 vya maji ya bomba vimejengwa.
Utunzaji wa vyanzo vya maji.
Katika jitihada za utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira yake, jumla ya miti 250 ilipandwa katika maeneo ya vyanzo vya maji. Pamoja na utunzaji wa vyanzo vya maji Sheria Ndogo Ndogo za uhifadhi wa mazingira zimetungwa ambapo mchakati wake upo katika hatua za kusainiwa. Pia elimu ya mazingira imetolewa katika vijiji 20.
Usambazaji na upatikanaji wa maji.
Katika kipindi hiki cha Awamu ya IV hadi kufikia Juni 2008, jumla ya watu 28,600 wamepatiwa huduma ya maji safi ambayo ni swa na asilimia kumi na tatu (13%).
Kamati za Maji na Mifuko ya Maji.
Kamati za vikundi vya watumiaji maji 98 katika vijiji 22 zimeundwa na kupewa mafunzo ambavyo vina Kamati za Maji.Aidha kamati hizi zimepewa amafunzo ya uendeshaji na matengenezo kwa lengo la kufanya miradi ya maji kuwa endelevu kwa vizazi vilivyopo na vijavyo.
 
Changamoto.......
http://www.morogoro.go.tz
 
 
Trekta la kijiji cha Usangule katika Wilaya Ulanga, moja ya matrekta 3 yaliyonunuliwa chini ya mradi wa PADEP
 
 
AFYA
Idara ya afya imeendelea kutoa huduma za afya ya tiba na afya kinga kwa wagonjwa wa nje wakiwemo wajawazito na watoto chini ya miaka mitano (5) wanaohudhuria kliniki na wagonjwa waliolazwa katika hospitali na vituo vya afya. Jumla ya vituo 35 vya kutolea huduma za afya katika wilaya vinaendelea kutoa huduma kwa wagonjwa na wateja wenye matatizo ya kiafya. Vituo hivyo vya tiba ni kama ilivyoonyeshwa katika jedwali.

Na. Aina Idadi Mmiliki
1 Hospitali 1 Serikali
2 Hospitali 1 KKKT
3 Vituo vya Afya 3 Serikali
  Zahanati 18 Serikali
    11 Jimbo Katoliki
    1 Binafsi
Jumla 35  
 

MMAM

Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga imeridhia tamko la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete sambamba na sera ya Taifa ya Afya , kuwa katika Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi kila kijiji kitajenga Zahanati na kila Kata itakuwa na Kituo cha Afya ili kuboresha na kufikisha huduma zote muhimu kwa wananchi wote.
Katika mpango huu wa Maendeleo ya Afya ya Msingi wananchi wa Wilaya wamehamasishwa vya kutosha kuhusu ujenzi wa vituo vya tiba hususan Zahanati na Vituo vya Afya. Aidha ujenzi wa Zahanati unaendelea katika vijiji vitano (5) vya Nakafulu, Chikuti, Isyaga, Ngombo na Kiswago ikiwa ni pamoja na nyumba za waganga kwa vijiji vinne vinavyojenga zahanati. Kwa mwaka wa fedha 2008/2009 kijiji cha Isongo pia kimetengewa fedha kwa ajili ya ujenzi wa zahanati na kijiji cha ngombo ujenzi wa nyumba ya Mganga. Kati ya vijiji hivyo jumla ya vijiji 18 vina Zahanati zinazomilikiwa na Serikali.
 
 
Changamoto
•  Upungufu wa wataalam wa Kada mbalimbali za Afya.
•  Uchakavu na ubovu wa majengo ya kutolea huduma kwa Vituo vingi vya tiba.
•  Up ungufu wa madawa na vitendea kazi katika Vituo vya tiba.
•  Ubovu wa uchakavu wa miundo mbinu katika Wilaya.
•  Mwamko mdogo wa jamii na kupungua kwa ari ya kuchangia huduma za Afya.
Upungufu wa mgao wa fedha za ruzuku katika Idara
 
 
 
Barabara
Hali ya barabara katika Wilaya ya Ulanga inaweza kuelezwa kwa kifupi kwa mchanganuo ufuatao:-
•  Urefu wa barabara yenye lami nyepesi ni Km. 3 katika mlima Ndororo
•  Urefu wa barabara zenye changarawe ni Km. 233.10
•  Urefu wa barabara za udongo ni Km. 586.59
Jumla ya urefu wa barabara ni Km. 822.69.
Utekelezaji wa kazi ya kuboresha barabara kwa kipindi cha mwaka 2006-2007/2007-2008:
Katika kipindi cha mwaka 2006-2007/2007-2008, Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga imefanya kazi za matengenezo ya barabara, ukarabati na ujenzi wa barabara mpya ili kutimiza Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2005

Malengo:
•  Kuendelea kutunza barabara tulizonazo ili ziendelee kuwa katika hali nzuri kwa kufanya matengenezo ya kawaida ya barabara na kufanya matengenezo ya maeneo korofi.
•  Kuboresha barabara za udongo na kuwa za changarawe kwa kufanya matengenezo ya muda maalum.
•  Kuendelea kuandika Maandiko mabalimbali ya kuomba fedha kwa ajili ya Ukarabati wa barabara zilizopo katika hali mbaya.
•  Kuendelea kuandika maandiko mbalimbali ya kuomba fedha kwa ajili ya kufungua barabara mpya kwa Vijiji na Vitongoji visivyofikika, pia kuwashawishi wananchi wa vijiji husika kutumia fursa ya Miradi ya TASAF, PADEP, VTTP n.k. kuibua Miradi ya barabara ili kuboresha sekta ya usafiri na usafirishaji.
 
 
Hifadhi ya Mazingira
Upandaji miti: -
Ofisi ya Maliasili (W) imeweza kutoa hamasa kwa wanavijiji kutenga maeneo kwa ajili ya kuanzisha mashamba ya miti. Watu binafsi na asasi zisizo za kiserikali zimehusishwa katika suala zima la upandaji miti hapa wilayani.
Kijiji cha Isongo kupitia mradi wa PADEP kimeweza kutenga eneo la kupanda miti 100,000 aina mbalimbali na bado wanaendelea. Mkakati ukiwa ni kufikia miti 200,000 ifikapo mwaka 2009.
Mikakati katika suala la upandaji miti:
Ili kuhakikisha kuwa zoezi la upandaji miti linatekelezwa ipasavyo, Idara ya Ardhi, Maliasili na Mazingira Kitengo cha Misitu, kina mkakati wa kuanzisha mfuko maalum wa upandaji miti ambapo kila mteja anayejihusisha na biashara ya mazao ya misitu atatakiwa kuchangia upandaji miti isiyopungua 100,000.
Wilaya ina mpango wa kuanzisha mashindano ya upandaji miti. Mashindano hayo yatavihusisha vijiji, watu binafsi, taasisi kama vile shule, Magereza na vikundi vinavyojihusisha na Hifadhi ya Mazingira hapa wilayani. Zawadi mbalimbali zitatolewa kwa washindi.
Utunzaji wa vyanzo vya maji: -
Wilaya ya Ulanga kwa kushirikiana na Serikali Kuu inatunza Misitu 8 ya Hifadhi (Catchment forests). Misitu hiyo ndiyo chanzo kikuu cha maji kwa wakazi wa wilaya ya Ulanga. Misitu hii ina ukubwa wa hekta 8,582

Halmashauri kwa kupitia Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu (Participatory Forest Management) vijiji vya Lukande, Chikuti, Kichangani na Kalengakero vimeweza kutenga misitu yao yenye ukubwa wa hekta 4,408. Kazi ya kutenga misitu katika vijiji vya Mdindo na Makanga inaendelea
Ili kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika kulinda na kuendeleza vyanzo vya maji, vijiji vya Vigoi, Nawenge, Isongo, Epanko, Makanga, Mdindo, Chikuti na Mzelezi vimo katika Mpango wa Pamoja wa Kulinda na Kuendeleza Misitu ya Hifadhi ya Serikali Kuu (Joint Forest Management).


Ardhi


Mpango wa matumizi bora ya ardhi
Jumla ya vijiji vitano vimeshaandaliwa mpango wa matumizi bora ya ardhi kupitia Participatory Land Use Management (PLUM). Vijiji hivyo ni Madibira, Kalengakero, Kipenyo, Kiswago na Usangule. Mpango huu utawezesha kila mwananchi kumilikishwa eneo lake na kupewa hati miliki. Aidha, zoezi hili litasaidia sana kuondoa kero ya migogoro baina ya wakulima na wafugaji na kufanikiwa kutekeleza moja ya Ilani ya Chama Tawala ya mwaka 2005.
Aidha kupitia mradi wa RAMSAR ambao unafanya kazi zake katika bonde la mto Kilombero unaozingatia matumizi bora na uhifadhi wa mazingira katika ardhi oevu utasaidia kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji. Mradi huu umeanza kufanya mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji tisa vya wilaya ya Ulanga ambavyo ni Madibira, Kipenyo, Itete Njiwa, Itete Minazini, Iragua, Milola, Mavimba, Minepa na Kivukoni.
 
Mifugo

Utangulizi
Wilayani Ulanga shughuli za ufugaji zimegawanyika katika mifumo miwili,ambayo ni shadidi na huria. Ufugaji shadidi unachukua sehemu kubwa katika ukanda wa juu hasa Tarafa ya Vigoi, ufugaji huria unafanyika kwa kiasi kikubwa katika ukanda wa chini, yaani katika Tarafa ya Lupiro, Mtimbira na Malinyi. Ufugaji huu unaochukua sehemu kubwa Wilayani na ndio chanzo kikuu cha nyama, ngozi na maziwa kwa kiasi kidogo
Hali ya malisho na maji
Kutokana na kuwepo kwa misimu miwili ya mvua wilaya ya Ulanga huwa inakuwa na malisho na maji ya kutosha kwa mwaka mzima ila upungufu kidogo hutokea kipindi cha mwezi Agosti – Oktoba.
Utengaji wa Maeneo ya Wafugaji
Kupitia mpango wa matumizi bora ya ardhi, jumla ya vijiji 5 vimetenga maeneo ya ufugaji kati ya vijiji 19 vilivyotambuliwa kuwa na mifugo.
Huduma za mifugo
Aidha huduma mbalimbali za ushauri wa mifugo na mazao yake zimeendelea kutolewa Wilayani. Huduma hizo ni;
•  Uzuiaji wa kupe
•  Tiba ya magonjwa
•  Kinga ya magonjwa
•  Usafi na ukaguzi wa nyama
•  Minada ya mifugo
•  Ushauri kwa wafugaji
Uogeshaji wa mifugo
Uogeshaji kwa ajili ya kuzuia magonjwa yaenezwayo na kupe umefanyika kwa njia ya kunyunyizia na mtumbukio kwa kutumia josho jipya lililopo katika kata ya Itete
Huduma nyingine za mifugo zitolewazo ni pamoja na:
•  Utoaji wa madini ya chuma (Iron Dextrose)
•  Kung'oa pembe
• Usafi na ukaguzi wa nyama



Uvuvi:
Sehemu kubwa ya uvuvi wilayani Ulanga hufanyika kutokea kwenye kambi za wavuvi zaidi ya 30 kando kando ya Mto Kilombero. Uvuvi mwingine (kwa kiwango kidogo) hufanyika katika mabwawa ya asili - zaidi ya 11 pamoja na mito imwagayo maji yake katika bonde la Mto Rufiji (Tarafa ya Mwaya).
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na WWF mwaka 1992 mavuno ya samaki yalikisiwa kuwa kati ya tani 9,500 na 12,000 kutoka mto Kilombero (Ulanga na Kilombero).
Sensa ya mwisho ya Uvuvi iliyoendeshwa mwaka 1997 ilibainisha kuwepo kwa wavuvi 2,500 wakati huo.
 
Ufugaji nyuki
Ufugaji nyuki katika Wilaya ya Kilombero umekuwa na mwitikio mkubwa kwa mtu mmoja mmoja na vikundi. Kuna jumla ya mizinga elfu nne (4000) katika Wilaya. Mizinga 500 kati ya hiyo ni ya kisasa na 3500 ni ya Asili. Kuna jumla ya vikundi 25 vya wafugaji nyuki vilivyoanzishwa hapa Wilayani.

3 comments:

  1. Ninakushukuru kwa maelezo yako mazuri, lakini maboresho zaidi yafanyike kuhusu sensa iliyofanyika hivi karibuni, ASANTE KARIBU MTIMBIRA

    ReplyDelete
  2. Asante kwa taarifa nzuri. Napendekeza ujaribu ku - update ziweze kwenda na wakati. Pia elezea fursa zilizopo Ulanga hususani kilimo

    ReplyDelete